CAG ANA WAJIBU NA MAJUKUMU GANI?

                                                                                                                                        Na. MED News.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na marekebisho yake ya mwaka 2005; katika Ibara ya 143 pamoja na kifungu Na. 10 (1)cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya Mwaka 2008 vinataja na kufafanua wajibu na Majukumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali 
Prof. Mussa J. Assad (aliyesimama)wakati wa ufunguzi wa 
Warsha ya Asasi Zisizo za Kiserikali iliyofanyika Dodoma, 2017

Majukumu na matakwa hayo ya Sheria ndiyo yanayompa CAG uwezo wa kufanya ukaguzi katika mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mikoa yote ya Tanzania bara na kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 45 (1) cha Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ya Mwaka 1982 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2000. 

Katika kutekeleza majukumu yake ya kisheria; Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anatakiwa na sheria zilizotajwa hapo juu kuzikagua na kuzitolea hati Halmashauri zote nchini. Kazi hii ya ukaguzi hutekelezwa kupitia ofisi za CAG zilizo katika mikoa yote ya Tanzania bara. Ofisi za Ukaguzi katika ngazi za Mikoa zinasimamiwa na wakaguzi wakuu wa nje Mikoa, na chini yao wanakuwa na wakaguzi ambao hufanya kazi za ukaguzi kwa timu.

Timu za ukaguzi huanza kazi mara tu Halmashauri zinapofunga hesabu zake za Mwaka tarehe 30 Juni kila mwaka. Baada ya ukaguzi wa mapato, matumizi na vitabu vya mwisho vya hesabu, wakaguzi hutoa taarifa ya awali ambayo mkaguliwa anatakiwa kuijibu ndani ya siku 21 kama inavyotakiwa na kanuni Na. 86 (2) ya mwaka 2009 ya kanuni za ukaguzi wa utumishi wa umma. 

Baada ya CAG kukabidhiwa taarifa hiyo na hoja zilizopatiwa majibu kamilifu kufutwa; zile ambazo hazikujibiwa huingizwa katika taarifa ya mwisho ya ukaguzi. Taarifa hii ya mwisho baada ya kusainiwa; taarifa ya pamoja huandaliwa na kuwasilishwa kwa Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya tarehe 30 Machi kwa ajili ya kuwasilishwa Bungeni.

Mwenyekiti wa Warsha Mr. E. Mbogo akiongoza
majadiliano ya wana warsha.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAG; Mwaka wa fedha ulioishia 2016 Juni, jumla ya Mamlaka za Serikali za Mitaa 171 zilikaguliwa na kupewa hati. Hata hivyo taarifa inaongeza kuwa Halmashauri 138 ambazo ni sawa na asilimia 89.2 zilipata hati za kuridhisha, asilimia 10.1 ya Halmashauri hizo ambazo ni 32 zilipata hati zenye shaka na Halmashauri 1 ambayo ni sawa na 0.4 asilimia ilipata hati isiyoridhisha.


Ofisi ya CAG imezitaka asasi za kiraia kote nchini ziisaidie serikali katika kusambaza taarifa za ofisi yake kwa wananchi na kuhakikisha kuwa asasi hizo zinazingatia usahihi wa taarifa wanazozipeleka kwa wananchi ili kuondoa mtafaruku kwao. 

Wana warsha waliiomba ofisi hiyo kutoa nakala zenye lugha rahisi zaidi kwa wananchi ili wasipate shida katika kusoma na kutafsiri taarifa hizo. Aidha washiriki wote walikubaliana kushirikiana na CAG na Ofisi za serikali za mitaa katika kutoa elimu kwa umma juu ya taarifa zinazotolewa na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. 
Ukaguzi Shirikishi huongeza chachu ya Uwajibikaji kwa Jamii




CAG ANA WAJIBU NA MAJUKUMU GANI? CAG ANA WAJIBU NA MAJUKUMU GANI? Reviewed by Unknown on October 05, 2017 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.