Tarehe 6 Desemba 2017 familia ya Jackson Ndeekia Makundi ya Mamba Komakundi inahitimisha siku ya 30 tangu kijana wake mpendwa Humphrey Jackson Makundi atoweke duniani kwa kifo cha kutatanisha. Humphrey Makundi alitoweka katika shule alikokuwa akisoma ya Scholastica iliyoko katika mji mdogo wa Himo Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Mnamo tarehe 7/11/2017 mwili wake uliokotwa katika mto Ghona umbali wa mita 300 kutoka ilipo shule ya Scholastika japo awali haukutambuliwa kuwa ni Humphrey na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi. Familia ya Makundi ilijulishwa na uongozi wa shule kuhusu kupotea kwa Humphrey shuleni hapo tarehe 8/11/2017 na juhudi za familia kumtafuta zilianza mara moja.
Baba na wana ndugu waliungana na kwenda katika shule ya Scholastica kwa ajili ya kupata taarifa za kina pamoja na kuongeza nguvu ya kumtafuta kijana Humphrey. Kwa mujibu wa maelezo ya uongozi wa shule ilionekana kuwa Humphrey aliondoka shuleni kwa kuaga kuwa anakwenda kwenye matibabu ya jino kwa kumuaga kiranja mkuu tofauti na utaratibu wa kuaga kwa walimu. Hata hivyo kuaga kwa utaratibu au la halina tatizo; muhimu niwapi aliko Humphrey. Majibu ya uhakika hayakupatikana zaidi ya kupeana moyo kuwa atarejea.
Familia iliongeza juhudi za uchunguzi na kufuatilia kila aina ya tetesi na kubaini kuwa yawezekana kuwa aliyeokotwa katika eneo la mto Ghona ni Humphrey; familia ilifanya jitihada kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi lakini kwa hali ya kustajabisha mnamo tarehe 12/11/2017 maiti ya Humphrey iliondolewa na Manispaa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Mawenzi na kuzikwa katika makaburi ya Karanga kwa madai kuwa haikuwa na ndugu. Hii inamaanisha kuwa maiti hiyo ilikaa pale Mawenzi kwa muda wa chini ya siku 7 na kuzikwa bila ya kuwepo kwa matangazo ya kina kwa jamii na hata kuhusisha familia iliyopotelewa na mtoto huyo.
Pamoja na kuzikwa kwa Humphrey tarehe 12/11/2017; taarifa tata kuhusu mwili wa aliyezikwa na Manispaa zilitia shaka. Taarifa za daktari zilieleza kuwa aliyezikwa alikuwa mtu mzima (35) mwenye ndevu na ambaye kifo chake kilitokana na maji. "Jambo ambalo si la kweli" Hali hii iliongeza nguvu na ari ya familia kufanya ufuatiliaji. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro nalo lilitoa ushirikiano kwa wana familia na kuwatia moyo katika kufanikisha uchunguzi.
Familia iliomba kibali cha kuufukua mwili huo ambapo siku tano baadae (17/11/2017) mwili huo ulifukuliwa kwa ajili ya utambuzi wa familia. Familia ilibaini kuwa aliyezikwa katika kaburi hilo ni Humphrey Jackson Makundi mwenye umri wa miaka 16, asiye na ndevu na ambaye kifo chake kilitokana na kipigo kwani alikuwa na jeraha kichwani la kupigwa na kitu kizito na kuvunjika mbavu 2 za kushoto. Shaka iliongezeka katika waliohusika na kuuokota mwili, kuhifadhi hospitalini, kuuzika na kutoa taarifa. Kwakuwa suala hilo liko mahakamani tuishie hapo. Hizo ni siku tano za Humphrey Katika kaburi la Manispaa ya Moshi.
Tarehe 6/12/2017 tunapohitimisha siku 30 za kifo na siku 4 za Humphrey baada ya maziko ya familia, tunalichukulia suala hili kuwa ni funzo kubwa katika jamii yetu na hususan wazazi wenye watoto katika shule za bweni na hasa binafsi kuchukua hatua za kina dhidi ya usalama wa watoto wao wawapo shuleni.
SIKU 30 ZA KIFO CHA HUMPHREY; SIKU 5, ZA MANISPAA NA SIKU 4 TANGU AZIKWE NA FAMILIA
Reviewed by Unknown
on
December 06, 2017
Rating:
No comments: