MTOTO ANA HAKI YA KUAJIRIWA?

                     
                         Na. MED News 
Mtoto ni Mtu aliye na Umri chini ya Miaka kumi na Nane
Sura ya 8 ya Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 inatambua haki ya Mtoto kufanya kazi. Sheria inasema kuwa Mtoto atakuwa na haki ya kufanya kazi nyepesi; Sheria inaongeza kusema kuwa kwa madhumuni ya kifungu kidogo cha (1)' umri wa chini unaoruhusiwa kwa Mtoto kuajiriwa ni miaka kumi na nne. 
Moja kati ya ajira zinazohusisha watoto.

Mtoto anaweza kuajiriwa isipokuwa lazima mwajiri ahakikishe kuwa anampangia Mtoto huyo kazi nyepesi za kufanya ili kulinda hadhi na haki ya Mtoto. Kwa mujibu wa Sheria hiyo ni kwamba "Kazi nyepesi" zinazotamkwa na sheria hii ni kazi ambazo haziwezi kuwa na madhara kwa afya ya Mtoto au maendeleo yake. Aidha kazi hizo ziwe ni zile ambazo hazimzuii wala kuathiri mahudhurio ya Mtoto shule, kushiriki katika shughuli za kujiendeleza kiufundi au programu ya mafunzo au uwezo wa Mtoto kunufaika na kazi za shule.

Pamoja na sheria kuruhusu ajira kwa Mtoto; Sheria imeweka katazo la "Kuruhusu kazi za kiunyonyaji" Sheria inakataza kumuajiri au kumshughulisha Mtoto katika aina yoyote ya kazi za kiunyonyaji. Sheria inasisitiza kuwa kila mwajiri ahakikishe kuwa kila mtoto aliyeajiriwa kihalali au kuajiriwa kufuatana na Sheria ya Mtoto na. 21 (2009) analindwa dhidi ya kutengwa na pia dhidi ya matendo yanayoweza kuwa na athari mbaya kwake kwa kuzingatia umri na uwezo wake.

Kazi za kiunyonyaji kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ni pamoja na zile zinazomnyima Mtoto fursa ya kupata afya njema au maendeleo, kazi ambazo zinamlazimu Mtoto kuzifanya kwa zaidi ya saa sita usiku, kazi ambazo hazifai kwa umri wake au Mtoto kutokupata malipo ya kutosha.

Iwapo mtu yeyote atavunja sheria katika kifungu hiki atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini isiyopungua laki moja (100,000) au kutumikia kifungo wa muda wa miezi mitatu au vyote kwa pamoja.

Katika kifungu B cha Sheria hii; Mtoto hataajiriwa au kuhusishwa na katika mkataba wa huduma ambayo itamhitaji afanye kazi usiku. Kazi ya usiku inatafsiriwa kuwa ni ile inayomhitaji Mtoto awe kazini kati ya saa mbili jioni na saa kumi na mbili asubuhi. 

Ikiwa mtu yeyote atavunja sheria katika kifungu hiki; atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini isiyopungua shlingi laki moja (100,000) au kutumikia kifungo jela kwa kwa muda wa miezi mitatu au vyote kwa pamoja.

Sehemu ya D ya Sheria hii inakataza ajira za lazima kwa Mtoto. Sheria inasema "Mtu yeyote anayemshawishi, atakayempeleka, atakayemtaka, au atakayemlazimisha Mtoto kufanya kazi kwa lazima atatenda kosa."


MTOTO ANA HAKI YA KUAJIRIWA? MTOTO ANA HAKI YA KUAJIRIWA? Reviewed by Unknown on October 08, 2017 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.