MED YASHAURIWA KUWAFIKIA WANANCHI VIJIJINI


Viongozi wa serikali za vijiji vya Ibugule na Mapanga katika kata ya Ibugule Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma; wamelishauri shirika la Marafiki wa Elimu Dodoma (MED) kuwafuata wananchi katika ngazi za vijiji na vingoji ili kuwaelimisha.
Wakiongea katika mrejesho wa taarifa ya utafiti wa hali ya Unyanyasaji wa Kijinsia katika Elimu ya Wasichana Wilayani Bahi viongozi hao wamekiri kuwepo kwa changamoto nyingi zinazo wanyima wasichana fursa ya kupata elimu sawa na wavulana.
Mradi wa kutatua changamoto za unyanyasaji wa kijinsia katika elimu kwa wasichana unatekelezwa na MED katika kata tatu za Bahi ambazo ni Ibugule, Chibugule na Mwitikila. Walengwa katika mradi huo ni wanafunzi wa kike wenye umri kati ya miaka 13-19 wa shule za Msingi na Sekondari za Ibugule, Chibelela na Mwitikira. Wasichana wa shule za msingi watakao nufaika na mradi huu ni katika shule za Mapanga na Isangha.

Jumla ya wanafunzi 250 wanatarajiwa kufikiwa moja kwa moja na mradi ambapo pia viongozi wa serikali za vijiji watakao fikiwa ni 125. 

Mradi huu unaofadhiliwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) kwa thamani ya TZS. 10,000,000= ni matokeo chanya ya mtangulizi wa mradi huo shirika la The Foundation for Civil Society (FCS) ambao walianza kutoa ufadhili katika Wilaya za Bahi na Kondoa toka mwaka 2016.

Kwa mujibu wa Mkurugezi Mtendaji wa MED Bw. Davis Makundi; lengo la Mradi huo ni kuboresha uwezo wa wasichana katika kupata Elimu na huduma za kielimu kwa kuwawezesha wasichana na wanawake kupaza sauti zao dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na kusikilizwa.
Viongozi hao wameshauri kuwa pamoja na kuwa na fursa ya kupata elimu wao; bado shirika lijitahidi kuweka utaratibu wa kuwafiiwa wananci katika mikutano yao ya hadhara hususan ile ya kisheria ili wapate elimu kwa pamoja. "Ninyi mkifika kwenye mikutano na kuongea mtasikilizwa kuliko sisi viongozi ambao kwanza wametuzoea na wakati mwingine tunashiriki kuwanyanyasa wanawake bila kujua" Alisema mmoja wa viongozi hao.

Wilaya ya Bahi ni miongoni mwa Wilaya ambazo wanafunzi wa kike wanaishi kwenye mageto kutokana na ukosefu wa mabweni pamoja na shule zao za sekondari za kata kuwa mbali na makazi ya wanavijiji.




MED YASHAURIWA KUWAFIKIA WANANCHI VIJIJINI  MED YASHAURIWA KUWAFIKIA WANANCHI VIJIJINI Reviewed by Unknown on September 29, 2017 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.