ATOA NG'OMBE 30 ILI AOZWE MWANAFUNZI

Hata kwa ng'ombe 100 bado  kwa umri ni Mtoto
Na.MED News.
Safari ya Tumaini Msowoya katika kubaini changamoto za Elimu kwa wasichana katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma inakutana na vigingi vya aina yake. Hakati tamaa; bado ana matumaini makubwa ya kufanikiwa. Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.co.tz


Kwa ufupi
“Sisi tulichokitaka ni mwanamke, tulimpa baba yake ng’ombe 30 tukamchukua, hivyo huyu siyo mtoto ni mkubwa tu.” Ilikuwa sauti ya mwanamke aliyekuwa ameongozana na wasichana wawili ambao kwa makadirio mmoja ana umri wa miaka kati ya 13 na 14 na mwingine 15 au 16.

Nilikutana nao katika Kijiji cha Chikola, Tarafa ya Chipanga wakati nikienda kwenye kata za Chali na Chifutuka zilizopo umbali wa takriban kilometa 120 kutoka makao makuu ya Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma. Baadaye nilikuja kubaini kwamba wasichana hao walikuwa wakifuata ng’ombe malishoni.

Kilichosababisha nimuombe mwendesha pikipiki kusimama ili niweze kuzungumza nao ni muda wa saa 3 asubuhi ambao kwa kawaida mabinti hao walipaswa kuwa shuleni wakisoma. “Habari za leo?” Niliwaamkia huku nikishuka kwenye bodaboda. Hakuna aliyejibu salamu yangu. Sikukata tamaa niliwaamkia kwa mara nyingine huku nikiwasogelea. Wakati huo walikuwa wamesimama wakinishangaa.

Niliwaamkia mara ya pili bila majibu, niliamua kuwageukia mabinti. “Hamjambo watoto wazuri?” Walinijibu: “Hatujambo, shikamoo”. Ghafla mama yule aliyekuwa nao aliingilia kati. “Huyu siyo mtoto ni mkubwa labda huyu mwingine, yeye ndiyo mtoto,” alisema huku akionyesha kwa kidole, yupi mtoto na yupi mkubwa kati ya mabinti wale wawili.

Majibu yake yalinipa hamu ya kutaka kujua zaidi kulikoni msichana anayeonekana kuwa ni mtoto aitwe mkubwa? Nilijiuliza, mbona mimi namuona kama mtoto? Niling’ang’ania kujua kwanini anamuita mtoto ni mkubwa, baadaye mama yule aliweka wazi akisema: “Huyu ameshaolewa tena kwa sherehe. Ni mkubwa sasa.”

Nilimtazama kwa makini msichana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Mage Kayungilo, nikabaini kwamba tumbo lake ni kubwa, hivyo nilihisi kwamba ni mjamzito. Nikawaza, kumbe mtoto huyu anakabiliwa na majukumu ya ndoa. Mwanamke aliyekuwa ameongozana naye ni mama mkwe wake.

“Kijana wangu alimpenda, amemuoa na sasa wanaishi wote,” anasema mama huyo ambaye hakutaka kabisa kutaja jina lake. Binti huyo alitakiwa kuwa kidato cha kwanza mwaka huu, kwani alihitimu darasa la saba mwaka jana katika Shule ya Msingi Chiguluka na kufaulu kuingia kidato cha kwanza. Hata hivyo hakwenda sekondari na badala yake aliolewa.

Mage anasema: “Harusi yangu ilikuwa mwaka huu, ilikuwa nzuri na tulikula wali. Ila napenda sana kusoma.”Awali ilikuwa vigumu kuzungumza na binti huyo kwani alikataa hata kutaja jina lake na shule aliyosoma, lakini kadri mazungumzo yetu yalivyoendelea alikubali kuzungumza.

Baada ya kama dakika kumi za kuzungumza nao, waliamua kuondoka, nami nikaendelea na safari yangu. Mage kwa umri wake ambao ni kati ya miaka 14 na 15 hivi, alipaswa kuwa darasani kwani alifaulu mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kwenda kidato cha kwanza.

Ushauri
 Mama mwenye nyumba, aliyewapangisha baadhi ya wasichana katika Kijiji cha Magaga, Peris Matonya anasema aliacha shule akiwa kidato cha pili na akaolewa. Anasema maisha ya ndoa ameshayazoea na tayari ana watoto wawili. “Kama ningeendelea kusoma ningekuwa kidato cha tano,” anasema Peris na kuongeza: “Sikumaliza shule nikaolewa, huwa nawaambia hawa wasichana waliopanga kwangu wasome, wasituige sisi.” Anasema umaskini wa kipato unaoikabili familia yake usingekuwepo kama angebahatika kuendelea na masomo yake.

Sheria
 Marekebisho yaliyofanywa na Bunge mwaka jana katika Sheria ya Elimu ya 1978 yanaweka adhabu ya miaka 30 jela kwa mtu yeyote ambaye ataingia kwenye uhusiano wa kindoa na mwanafunzi yeyote wa shule ya msingi au sekondari.

Kifungu cha 60 A (4) kinatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela au faini ya Sh5 milioni au vyote kifungo na faini kwa kwa mtu yeyote ambaye atatiwa hatiani kwa kosa la kusaidia kufungwa kwa ndoa ya aina hiyo.

Kwa upande wa kifungu cha 60A (5) kinatoa fursa kwa vifungu vilivyoko kwenye kanuni za adhabu (penal code) vinavyohusiana na makosa ya kujamiiana kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18 pamoja na makosa yanayotajwa kwenye Sheria ya Mtoto ya 2009, kutoa adhabu sambamba na Sheria ya Elimu ikiwa kesi inamuhusisha mwanafunzi mwenye umri chini ya miaka 18.

Takwimu za afya na idadi ya watu nchini za 2016 zinaonyesha kuwa Mkoa wa Dodoma unashika nafasi ya nne kwa mimba za utotoni ukiwa na asilimia 51, nyuma ya ShinyanGa (asilimia 59), Tabora (58) na Mara 55.

Taasisi ya kimataifa ya Haki za Binadamu iitwayo Human Right Watch, katika ripoti yake iitwayo, ‘Nilikua na Ndoto ya Kumaliza Shule: Changamoto za Elimu ya Sekondari Tanzania’, inasema katika kila watoto watano wa kike nchini, wawili huolewa kabla ya miaka 18. Wilayani Bahi, Mwananchi liliambiwa kuwa ndoa za utotoni zimekuwa zikifungwa kwa siri, zikiwahusisha wanafunzi ambao hukatisha masomo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Makanda, Chonama Sekondari anasema udhibiti wa ndoa hizo unahitaji nguvu za ziada. “Ingekuwa wanafanya hadharani tungeweza kuwakamata, hivi juzi tu tulisika kuna harusi inaandaliwa, walipojua tumejua, wamesambaratika,” anasema.

Kauli yake inaungwa mkono na ile ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Bahi Sokoni, Macheti Mlyanzoka ambaye anakiri kwamba ndoa za utotoni zipo hata kwenye kijiji chake na zinafungwa kwa siri.

“Hii ni changamoto kubwa na kinachoumiza ni kwamba zinafungwa kwa siri,” anasema. Mwenyekiti huyo anataja Kitongoji cha Sanduli kuwa kinaongoza kwa ndoa za utotoni kati ya vitongoji 18 vya kijiji hicho.

“Mtaa wa Sanduli ndiyo wenye ndoa za utotoni zaidi, wazazi wanachotaka ni mahari tu na wakishaona wana watoto wa kike na wamekua huanza kuwarubuni waachane na masomo. Wanaamini mtoto wa kike ni mtaji,” anasema. Maneno ya mwenyekiti huyo yanashabihiana na yale ya mwanamke aliyekuwa na mabinti wawili, akijisifu kwamba walilipa ng’ombe 30 na kumchukua binti.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Chifutuka, Gasper Mhembano anasema: “Wanajua sheria haipo upande wao ndiyo maana hawazitangazi, sherehe zao wanafanya kwa siri na wanaotusumbua zaidi ni jamii ya wafugaji.” Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chifuduka, Daniel Mchomvu anathibitisha kwamba ameshakutana na kesi za wazazi kuwabembeleza watoto wao wa kike wakatae shule, lakini akasema tatizo ni usiri uliogubika vitendo hivyo.

Wasichana wafichwa
 Afisa Elimu Sekondari wilayani Bahi, Hassan Mohamed anasema uongozi wa halmashauri umelazimika ‘kuwaficha’ baadhi ya mabinti wanafunzi kama hatua ya kuwalinda wasiozeshwe na wazazi wao.

“Tumewaweka mahali wasikokutana na wazazi wao mpaka watakapomaliza mitihani,” anasema na kuongeza: “Tuna hakika watafaulu na watafaulu tu, sheria inawabana wazazi kuhakikisha wanaendelea kuwasomesha.” Anasema hatua ya kuwahifadhi ni kuwatenga na wazazi ambao wamekuwa wakiwashawishi wasizingatie kwenye mitihani ili waachane na masomo.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Chikopelo, Cornelius Mahinyila anasema ndoa za utotoni zipo japo wengi wanaoolewa ni wale walioacha shule au kutoanza kidato cha kwanza licha ya kufaulu.

“Kuna msemo wazazi huwa wanawaambia watoto wao ‘nenda kayakoroge’ ili wakiacha shule na kurudi nyumbani aolewe,” anasema. Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Sekondari Magaga, Jaliwa Mahenge anasema mipango ya kuacha shule hupangwa kati ya wazazi na wanafunzi.

Kaimu Ofisa Elimu Taaluma wa Shule ya Msingi wilayani Bahi, Grace Samwel anasema matajiri wa ng’ombe ni miongoni mwa watu hatari kwa watoto wa kike. “Mtoto wa kike anaweza kuwa na uwezo mzuri darasani, tajiri ng’ombe akamrubuni anaacha shule baadaye anaolewa huko,” anasema.


Anasema mwamko mdogo kuhusu elimu hasa kwa mtoto wa kike ndiyo unaosababisha watoto wa kike kuolewa kwenye umri mdogo.
ATOA NG'OMBE 30 ILI AOZWE MWANAFUNZI ATOA NG'OMBE 30 ILI AOZWE MWANAFUNZI Reviewed by Unknown on November 21, 2017 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.