Tujitahidi kuwapa Elimu Bora badala ya Mimba
Unajua kinatokea nini katika kijiji cha Bahi Sokoni kilichoko Wilaya ya Bahi Mkoa wa Dodoma? Takwimu za mimba hizi hapa! Jiunge na Tumaini Msowoya wa Gazeti la Mwananchi upate undani wa suala hili.
TAKWIMU ZA MIMBA SI ZA KAWAIDA
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiahirisha kikao cha Bunge
mjini Dodoma Julai 5, 2017 alisema takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2015,
wanafunzi 3,637 waliacha masomo kutokana na tatizo hilo.
Tumaini Msowoya, Mwananchi; tmsowoya@mwananchi.co.tz Katika Wilaya ya
Bahi, mkoani Dodoma kipo kijiji maarufu kinachoitwa Bahi Sokoni.
Ni sehemu iliyochangamka kiasi kutokana na shughuli za
biashara za maduka ambazo zimeshamiri, huku wakazi wake wengine
wakijishughulisha na kilimo. Ni saa 12 na dakika kadhaa jioni, jua likielekea kuzama;
naingia katika mitaa ya kijiji hiki. Katika mtaa mmoja, nakutana na mashine ya kusaga nafaka. Nyuma
ya mashine ipo nyumba kuukuu.
Naitazama nyumba hii, nagundua kwamba hapa ndipo mahali
nilipoelekezwa. Ni makazi ya Mzee Ally Mohamed mwenye umri wa miaka 60. Baada ya kubisha hodi, ilisikika sauti ikiitikia “karibu”
huku mlango wa nyumba ukifunguliwa. Alijitokeza binti ambaye baadaye
alijitambulisha kwa jina la Mariam Ally. Uso wake umekunjamana na anaonekana
kama amezama kwenye lindi la mawazo.
Baada ya kunikaribisha na kuketi kwenye kiti kilichokuwapo
katika uwanja ulio mbele ya nyumba, napata hisia kwamba huyu ni binti ambaye
nilipata taarifa kwamba ameachishwa shule kutokana na kupata ujauzito. Baadaye
nilithibitisha kwamba hisia hizi zilikuwa kweli.
Mariam (17) alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika
Shule ya Sekondari ya Bahi. Wakati nafika kijijini kwake Agosti 15, 2017,
ilikuwa imepita siku moja tu tangu aache masomo kwa sababu ya ujauzito. Hili
ndilo lilimfanya aonekane mwenye huzuni. Huenda alikuwa akitafakari namna ya kuyakabili majukumu
mapya na mazito ya kulea mimba na baadaye ulezi wa mtoto. Hii ni
tofauti kabisa na malengo yake ya
kusoma.
![]() |
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kigwe Wilaya ya
Bahi wakipiga kura kuchagua viongozi wa Club ya Wasichana kwa
ajili ya lijadili changamoto za wasichana katika Elimu.
Picha na MED
|
Anasema walipopata taarifa za ujauzito wa mwanafunzi huyo,
walienda kumpima na alipogundulika walitoa taarifa kwa uongozi wa juu ikiwamo
ofisi ya kata na polisi. Mtendaji wa Kata ya Bahi, Juma Idd naye anakiri kupokea
taarifa hiyo na kwamba wanachofanya sasa
ni msako wa mwanaume aliyempa mimba msichana huyo ili sheria ichukue mkondo
wake.
Kanuni Namba 4 ya Kanuni za Elimu Toleo la 2002, inaelekeza
kufukuzwa shule kwa mwanafunzi yeyote wa kike na au wa kiume ambaye
anajihusisha na vitendo vya ngono. Mimba imekuwa ikitumika kama uthibitisho kwamba mwanafunzi
husika amejihusisha na vitendo hivyo.
Simulizi ya Mariam iko hivi;
Anasema ilikuwa likizo ya Desemba 2016, wakati alipokutana
na shemeji yake ambaye alimlazimisha kufanya mapenzi. “Shemeji yangu hajui kama
nina mimba, sijamwambia kwa kuwa sina mawasiliano naye. Yeye anaishi Dar es
Salaam na mimi nilienda kule likizo,” anasema.
Anasema wakati anasoma aliweza kupambana na kushinda
vishawishi alivyokuwa akikutana navyo, kwani alikuwa akitembea zaidi ya
kilometa tano kwenda na kurudi shuleni kila siku.
Anavitaja vishawishi hivyo kuwa ni pamoja na lifti za
waendesha pikipiki, lakini anaumia kwamba ameangukia katika mikono ya mtu
aliyepaswa kumlinda ambaye ni shemeji yake, mume wa dada yake.
Kisa cha Mariamu kinaakisi hali halisi ya elimu kwa watoto
wa kike ilivyo wilayani Bahi. Kwa mfano, katika
shule ya Sekondari ya Chikopelo wilayani humo, kati ya wanafunzi 67 walioanza kidato cha kwanza 2014, wamebaki
wanafunzi 26 wanaotarajiwa kumaliza kidato cha nne mwaka huu.
Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo, Ahadi Mgando anasema
walianza wasichana 31 lakini waliobaki ni 12 tu huku wengi wakiacha masomo kwa
sababu mbalimbali ikiwamo kupata ujauzito.
Mkurugenzi wa Shirika la Marafiki wa Elimu Dodoma, Davis Makundi anasema katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Babayu, wasichana sita
kati ya wanane waliokuwa kidato cha nne walipata mimba na kuacha shule mwaka
2015.
Kilio cha mzazi
Baba yake Mariam, Ally Mohamed (60) anasema hajui afanye
nini kwani suala la mwanawe kuwa mjamzito limemchanganya kiasi cha kuhisi kupata
ugonjwa wa moyo. “Nilijua binti yangu atamaliza masomo bila bugudha yoyote,
kwa kweli naumia sana, nimechanganyikiwa mno,” anasema na kuongeza: ‘‘Umekuja wakati tayari binti
yangu ameshaharibikiwa? Kwa nini huwa hamuwasaidii kabla hawajafikia hatua hii?
Inaniuma sana.”
Mzee Ally ambaye ndiye mlezi pekee wa Mariam, kama ilivyo
kwa binti yake huyo, anatamani mwanawe apate nafasi ya kuendelea na masomo
baada ya kujifungua. Hata hivyo, suala hilo haliwezekani kwani mbali na kikwazo
cha Sheria ya Elimu ya 1978 na Waraka wa Kanuni za Elimu wa 2002, Rais John
Magufulu ameweka msimamo kwamba hilo haliwezekani asilani katika uongozi wake.
Tatizo la wanafunzi
wasichana wanaoacha shule kwa sababu ya mimba pia ni kubwa katika mtazamo wa
kitaifa.Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiahirisha kikao cha Bunge mjini Dodoma
Julai 5, 2017 alisema takwimu zinaonyesha kuwa 2015, wanafunzi 3,637 waliacha
masomo kutokana na tatizo hilo.
Vichocheo vya mimba
Makundi anasema wasichana wengi wanajilea wenyewe katika
vyumba wanavyopanga kutokana na makazi yao kuwa mbali na shule wanazosoma. “Pia, kuna suala la mila na desturi za kutojali watoto wa
kike, kwamba wao ni wa kuolewa tu, hivyo kuna wakati wazazi wanaona mimba za
watoto hawa ni kitu cha kawaida,” anasema.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Matolee Festo Matonya anasema: “Wasichana wengi
wanaishi peke yao na wale wanaoishi kwa wazazi wanatembea umbali mrefu.
Unadhani nini kitakachotokea hapo? Ni vishawishi na mimba tu”.
Anaongeza: “Mfano
shule yetu ya Bahi, tatizo kubwa ni gharama za kukaa bwenini, inabidi watembee
umbali mrefu na njiani wanakutana vishawishi ikiwamo bodaboda wanaowarubuni kwa
chipsi.”
Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Magaga, Laurent John anasema
ili kupunguza tatizo hilo, lazima watoto wapewe malezi ya kimaadili na ujenzi
wa mazingira mazuri ya kusomea kwa wanafunzi.
Hatua za kudhibiti
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Elizabeth Kitundu anasema Serikali
haitamfumbia macho mwanaume yeyote atakayebainika kumpa mimba mwanafunzi na
kwamba, amewaelekeza wenyeviti wa vijiji kuwachukulia hatua, pia wazazi
watakaobainika kuwaficha wanaume waliowapa mimba watoto wao.
“Mimba ni changamoto
kwa watoto wetu, nimeshapita huko kote kuwasihi wanafunzi waachane na tamaa,
hayo yote watakayakuta huko mbele, wasome kwanza,” anasema.
Katika Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba
mbili ya 2016, Bunge liliridhia adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa mwanaume
atakayethibitika kujamiiana na mtoto wa kike mwenye umri wa chini ya miaka 18
akiwamo mwanafunzi.
Ofisa Elimu Sekondari wa Bahi, Hassan Mohamed anasema
wamewaagiza watendaji wa kata na vijiji kuwakamata wahusika wa mimba za
wanafunzi ili sheria ichukue mkondo wake.
“Sisi tunachofanya ni
kusimamia sheria, hata hivyo mimba kwenye wilaya yetu imepungua kwa kiasi
kikubwa, mwaka huu tumepata kesi chache tu,” anasema.
Katika shule aliyosoma Mariam, Mwalimu Stellah anasema ili
kukabiliana na tatizo hilo, wamekuwa wakizungumza na watoto wa kike na
kuwaambia ukweli kuhusu maisha na umuhimu wa kujitunza.
MIMBA ZAONGEZA KICHEFUCHEFU KWA WANAFUNZI WILAYA YA BAHI
Reviewed by Unknown
on
November 21, 2017
Rating:
![MIMBA ZAONGEZA KICHEFUCHEFU KWA WANAFUNZI WILAYA YA BAHI](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjsA9-XmT4fSriZlX1RAx28OsC0sU9vwh8zNlzHtaBWjca34wVknrzeELkP1nJK600WNitIKG6z5P1dw1YhuDsVl-9vmIbYUpCTecyy9hhHIl9uiuZK3Nrkn-Mzen8Ff6goxXoPcromWoEb/s72-c/IMG_20170802_134718.jpg)
No comments: